Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, kutokana na mnasaba wa kongamano la kutimiza miaka mia moja tangu kuanzishwa kwa Hawza ya Qom, mfululizo wa maandiko na mahojiano na wasomi wa Hawza na vyuo vikuu unachapishwa kwa lengo la kuelimisha na kutoa mwangaza kwa wanafunzi vijana na watu wa jamii kwa ujumla.
Ripoti fupi kutoka kitengo cha Fiqhi na Usūl kutoka kwa katibu wa kongamano la kutimiza miaka mia moja ya Hawza ya Qom, nukuhu ya Hujjatul Islam wal-Muslimīn Ithnā‘asharī, Mkurugenzi wa Ofisi ya Fiqhi Mu'asir Hawza ya Qom:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu
Kitengo cha Fiqhi na Usūl kilikuwa ni miongoni mwa vitengo muhimu vilivyoundwa kwa madhumuni ya kuchunguza mabadiliko ya kielimu katika Hawza ya Qom. Wajibu mkuu wa kitengo hiki ulikuwa ni kuchunguza mitazamo mahsusi na ubunifu wa mafuqahā mashuhuri wa Hawza ya Qom kwa mujibu wa orodha ya majina ya wakubwa iliyokuwa imetayarishwa hapo awali.
Jambo muhimu kuhusu fiqhi ni kuwa, kwa uwazi kabisa, fiqhi si taaluma inayopatwa na mabadiliko ya kimsingi katika muundo wake wa kimtazamo au katika maudhui yake. Bali fiqhi, kwa kutegemea njia na sunnah za kihistoria tangia miaka elfu moja, huchunguza masuala mapya na kutoa mitazamo kuhusu mambo hayo.
Kwa msingi huu, hatua ya kwanza ya kitengo cha fiqhi ilikuwa ni kuanzisha utafiti wa kina kwa ushiriki wa takriban watu kumi kutoka ngazi mbalimbali kuanzia wanafunzi, vijana waelewa, hadi walimu mashuhuri na watafiti wazoefu.
Katika mchakato huu, uchunguzi wa kina ulifanyika kuhusu mitazamo ya kifiqhi na kiusūl ya mafuqahā kama vile Ayatollah al-Udhma Būrūjirdī (r.a), Imamu Khumaynī (r.a), Ayatollah Shaykh Murtadhā Hā’irī (r.a), Ayatollah Dāmād (r.a), na Ayatollah Bahjat (r.a). Tulichunguza kwa pamoja makala zilizochapishwa kuwahusu wakubwa hawa na pia kazi halisi walizo ziandika hasa katika maeneo ya fiqhi, usūl na, kwa uchache, rijāl.
Mafuqah'a mashuhuri wa Qom, kwa maana mahsusi, pamoja na wakubwa waliotajwa hapo, kwa kawaida hupatwa na changamoto ya pamoja katika sekta ya utafiti: idadi ya watu wanaofahamu kwa kina mitazamo yao ya kitaalamu na wanaoweza kubainisha tofauti ya mitazamo hiyo na ya mafuqahā wengine au na kauli mashuhuri katika fiqhi ni wachache sana. Kwa sababu hii, utafiti wa kina na mpana ulikuwa muhimu. Sambamba na kusoma vyanzo, tulitumia pia ushauri na mwongozo wa walimu ili kuweza kugundua vyanzo muhimu na kuendeleza uchambuzi na ukamilishaji wa taarifa.
Mchakato huu wa utafiti uliendelea kwa muda wa takriban mwaka mmoja na nusu. Kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, hadi sasa kazi tano kamili zimeandaliwa, ambazo zitawasilishwa katika juzuu moja. Aidha, kuna uwezekano kwamba kazi nyingine kuhusu baadhi ya mafuqahā wa kisasa ambao mitazamo yao imekusanywa, zitajumuishwa pamoja.
Jambo la kuvutia na la kipekee katika mkusanyiko huu ni kuwa umeandikwa kwa muhtasari, kitaalamu na bila ya kupoteza muda mwingi. Ndani ya kazi hii, mitazamo ya wakubwa haikubainishwa kwa ujumla na kijumla, bali sehemu zile tu mahsusi na za ubunifu au angalau ambazo kwa wakati wao hazikuhesabiwa kuwa mitazamo ya kawaida. Lengo lilikuwa ni kuifanya mitazamo na kanuni za kipekee za mafuqahā hawa kuwa ni mwanzo wa uzalishaji mpya wa kielimu kwa watafiti na wanafunzi wa Hawza.
Kwa mfano, Ayatollah Būrūjirdī, tofauti na mtazamo mashuhuri, hawaoni kuwa dalili ya kimatamshi peke yake inatosha, bali wanasisitiza juu ya dalili ya kitendo. Vilevile, marehemu Imamu Khumaynī (r.a) ametoa tafsiri maalum na ya kitaalamu kuhusu hadithi ya ‘Umar bin Hanzala’ na dalili yake kuhusu wilāyat al-faqīh na dola ya Kiislamu.
Jambo la kuvutia ni kuwa Ayatollah Būrūjirdī pia anakubali dalili ya hadithi hiyo kuhusu wilāyat al-faqīh, lakini kwa maelezo tofauti.
Miongoni mwa mambo mengine ni mitazamo ya Ayatollah Shaykh Murtadhā Hā’irī. Yeye ni miongoni mwa mafuqahā ambao katika miaka ya hivi karibuni hawakujulikana sana, lakini kwa haki ni mtu mwenye mitazamo, mwenye kauli na mwenye uzalishaji wa kifiqhi. Kwa bahati mbaya, kazi zake zilichapishwa kwa kuchelewa, baadhi zilikusanywa na wanafunzi wake, na baadhi hata bado hazijawahi kuwasilishwa kwenye darsa khārij; kwa hivyo hadi leo hazijapewa umuhimu mkubwa na watafiti wa Hawza.
Tunatarajia kuwa kazi hii ya kielimu itakuwa ni mwanzo wa kuangaliwa kwa uzito zaidi mitazamo ambayo haijajulikana sana ya baadhi ya mafuqahā wetu wakubwa, mitazamo ambayo inastahili kupewa nafasi zaidi na zaidi na wanafunzi pamoja na watafiti wa Hawza.
Bila shaka, tija za kielimu zilizoachwa na Imamu Khumaynī (r.a), Ayatollah Būrūjirdī, Ayatollah Hā’irī na wakubwa wengine, ni hazina ya thamani kubwa kwa fiqhi ya zama hizi.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu aikubali hatua hii ndogo kutoka kwetu na aifanye kuwa ni kazi inayokubalika mbele ya hifadhi Yake.
Na shukran zinamstahiki Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe.
Maoni yako